Wanafunzi 76 wanusurika kifo bweni likiteketea Kibaha

Wanafunzi 76 wa shule ya Sekondari ya Wasichana Mkuza mjini Kibaha wamenusurika kifo baada ya moto uliozuka ghafla kuteketeza bweni la shule hiyo.

Dar es Salaam. Wanafunzi 76 wa shule ya Sekondari ya Wasichana Mkuza mjini Kibaha wamenusurika kifo baada ya moto kuteketeza bweni la shule hiyo.

Moto huo ambao uliozuka ghafla umeteketeza bweni la shule hiyo inayomilikiwa na Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani usiku wa kuamkia leo Jumatatu Mei 16, 2022.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ambaye alifika eneo la tukio amesema wanafunzi wote wako salama na Serikali imeshaunda timu ya wataalamu wa kuchunguza chanzo cha tukio hilo.

Kunenge amesema moto huo umetokea wakati wanafunzi wakiwa wameenda kwenye sala huku mmoja pekee ndio alikuwa amebaki bwenini.

“Woto watoto wako salama, wazazi na wananchi msiwe na wasiwasi, utaratibu utafanyika na watapata sehemu nyingine ya kukaa na wataendelea na masomo kama kawaida” amesema Kunenge

Amesema kuwa nguo na vifaa vyao vyote vimeteketea lakini wataendelea na masomo wakati utaratibu wa kuwapatia vifaa ukiendelea.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Alex Malasusa amewataka wanafunzi wasiwe na hofu na waendelee na ari ya kusoma.

Kwa upande wake Marakibu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani, Kamanda Jenifa Shirima amesema kuwa wamefanikiwa kuudhibiti moto huo usiteketeze mabweni mengine mawili ambayo yapo karibu na bweni hilo.

Kamanda Jenifa amesisitiza wananchi kutoa taarifa mapema za matukio ya moto ili uokoji ufanyike kwa wakati


Kinglayz Wakuchana

378 Blog posts

Comments