Jinsi ya kuishi na pumu ya ngozi bila madhara

Ugonjwa wa pumu ya ngozi ni wa kurithi na wataalamu wa afya wanasema mtu anaweza kuishi nao kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu bila ya kumletea madhara yoyote katika ngozi yake

Ugonjwa wa pumu ya ngozi ni wa kurithi na wataalamu wa afya wanasema mtu anaweza kuishi nao kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu bila ya kumletea madhara yoyote katika ngozi yake.

 

Dar es Salaam. Ugonjwa wa pumu ya ngozi ni wa kurithi na wataalamu wa afya wanasema mtu anaweza kuishi nao kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu bila ya kumletea madhara yoyote katika ngozi yake.

 

Ugonjwa huu unaweza kumtokea mtu katika umri wowote, hutokea kutokana na tofauti ya maumbile ya mtu ya ndani, vichocheo vya kimazingira na mpalaganyiko wa kinga za mwili.

 

Magdalena Dennis, Daktari Bingwa wa magonjwa ya ngozi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akizungumza na Mwananchi anasema kuna baadhi ya watu ugonjwa huu hujitokeza wakiwa wachanga, wengine wakiwa watoto kuanzia umri wa miaka miwili mpaka 12 na wengine kuanzia miaka 12 na kuendelea.

 

Pia wapo wanaobaini kuwa na ugonjwa huo hata wakiwa na umri wa miaka 60.

 

Hata hivyo, Dk. Dennis anasema moja ya vitu vinavyosababisha kutokea kwa ugonjwa huo ni maumbile ya mtu ya ndani ya mwili ambayo hutokea kuwa tofauti na watu wengine pamoja na vichocheo vya kimazingira.

 

Anasema vitu vya kimazingira vinavyochochea kutokea kwa ugonjwa huu ni matumizi ya sabuni na manukato yenye harufu kali, hasa marashi.

 

“Pia mabadiliko ya hali ya hewa ni kichocheo, mfano ikiwa joto au baridi sana inaweza kuchochea kutokea kwa ugonjwa huo kwa baadhi ya watu. Pia vipo baadhi ya vyakula vinaweza kuwa vichocheo kama ulaji wa aina nyingine ya samaki na mayai,” anasema.

 

Kwa upande wake, Daktari wa magonjwa ya ngozi katika Hospitali ya Temeke, Dar es Salaam, Claud Mango anasema sehemu kubwa ya pumu ya ngozi ni ugonjwa wa kurithi, lakini pia huchochewa na mparanganyiko wa kinga ya mwilli.

 

Anasema moja ya dalili ni kupotea kwa nyusi machoni, kutokwa na mikunjo chini ya jicho, baadhi ya watoto kuwa na nyama za pua, michirizi mikononi na miguuni.

 

Anasema kwa sasa ugonjwa wa pumu ya ngozi umeongezeka nchini, kwani kati ya wagonjwa 10 anaowapokea kwa siku, watano hugundulika kuwa na tatizo hilo.

 

Advertisement

“Kuna nchi duniani wagonjwa wa pumu ya ngozi wanafika mpaka asilimia 40, ugonjwa huu kwa hapa kwetu unaongezeka kila kukicha na tatizo kwa sasa ni kubwa. Mimi naweza kusema kama asilimia 20 ya Watanzania wanaweza kuwa wanaugua magonjwa ya ngozi,” anasema Dk. Mango.

 

Vitu wanavyokatazwa kufanya

 

“Tunatoa maelekezo ya namna ya kuishi nao, ikiwemo kuwakataza kuoga maji ya moto, baridi kwa hiyo maji yao yanatakiwa yawe ya kawaida,” anasema.

 

Anasema pia wanawakataza kukaa bafuni kwa muda mrefu na kuongeza kuwa wanatakiwa kukaa dakika zisizozidi tano kama wasipojali.

 

“Wakiingia bafuni wanatakiwa kuoga ndani ya dakika tano, tunawasitiza wasitumie sabuni kama hakuna ulazima wa kufanya hivyo, ila kama wakitaka kutumia basi zitumike zile ambazo hazina harufu kali,” anasema.

 

Dk Mango anasema akitoka bafuni haruhusiwi kujifuta au kujikausha maji kwa taulo, kwani akifanya hivyo atatengeneza muwasho utakaomfanya ajikune na kumletea shida katika ngozi yake.

 

Aidha, anasema kuwa mtu mwenye pumu ya ngozi anapaswa kuepuka kutumia mafuta yenye kemikali nyingi na manukato yenye harufu kali.

 

Pia wanatakiwa kuepuka kucheza na wanyama wenye manyoya, kwani wana uwezekano mkubwa wa kuchochea kutokea kwa ugonjwa huo katika miili yao.

 

Kwa upande wa mavazi, Dk. Mango anasema mtu mwenye pumu ya ngozi anatakiwa kuacha kuvaa nguo za mpira, kuteleza, lesi badala yake awe anavaa nguo zilizotengenezwa kwa pamba.

 

Dalili zake

 

Pumu ya ngozi ni ugonjwa unaoshambulia ngozi na kuifanya kuwa kavu, kuwasha na kupata vijipele vidogo vidogo vyenye rangi nyekundu.

 

Dk Dennis anasema ugonjwa huo una dalili tatu ambazo ni ngozi kuwa kavu, kuwasha na baadaye kuanza kutoa vipele vya aina tofauti.

 

“Katika suala la ngozi kuwa kavu tumekuwa tukiwashauri wagonjwa kupaka mafuta ambayo hayana manukato, ambayo ni ya nazi, mzaituni, mchikichi na mnyonyo. Hayo yote ni salama na hayana harufu kali,” anasema.

 

Anasema mtu mwenye ngozi kavu anashauriwa kupaka mafuta mara kwa mara kila baada ya saa moja hadi mawili au ikiwezekana zaidi ya hapo.

 

Dk. Dennis anasema kwa upande wa ngozi kuwasha inatokana na kuwa kavu, hivyo wanashauri mtu awe na tabia ya kupaka mafuta mara kwa mara, ili kupunguza tatizo hilo.

 

“Pia kama ngozi itawasha zaidi, basi tunampatia dawa ya kupunguza muwasho,’” anasema.

 

Aidha, anasema kwa upande wa vipele hulazimika kuvitibu kwa kumpatia mtu dawa kulingana na aina ya vipele alivyokuwa navyo, kwani vipo vikavu na vibichi.

 

“Hata hivyo, ikumbukwe kwamba jinsi unavyokua na kuzoea mazingira, ugonjwa huu uweza kupungua au kupotea kabisa, unabakiwa na historia kuwa ulikuwa nao.

 

“Kwa sasa idadi kubwa ya wagonjwa wa pumu ya ngozi ni wanawake na dawa tunazowapatia huwa zinasaidia kupunguza maumivu fulani yanayotokana na kujikuna au ngozi kuwa kavu,” anasema.

 

 

 

Upo uwezekano wa kutibiwa?

 

Dk. Mango anasema upo uwezekano mkubwa wa mtu mwenye ugonjwa huo kutibiwa na kusahau kama alikuwa akisumbuliwa na pumu ya ngozi.

 

“Mgonjwa atapewa ushauri wa kitaalamu juu ya tiba na maelekezo jinsi ya kuishi nao,” anasema.

 

Dk Mango anasema mgonjwa wa pumu ya ngozi mwenye umri chini ya miaka miwili ana dawa yake ya kutumia na wale ambao ni zaidi ya miaka hiyo pia wana dawa zao.

 

“Kwa Tanzania zipo dawa za daraja la kwanza, pili hadi tatu, hivyo mgonjwa hupatiwa dawa kulingana na daraja alilopo,” anasema


Kinglayz Wakuchana

378 Blog posts

Comments