Hassan Sheikh Mohamud: Somalia yampata rais mpya - aliyechaguliwa na watu

Hassan Sheikh Mohamud atahudumu kama rais kwa kipindi cha miaka minne , akirudi katika jukumu lake aliloshikilia kati ya mwaka 2012 hadi 2017.

Uchaguzi huo ulishirikisha wabunge 328 pekee kutokana na suala la ukosefu wa usalama ambao huenda lingeathiri uchaguzi huo , huku mbunge mmoja akikosa kupiga kura.

 

Bwana Mohamud alipokea kura 214 , akimshinda Farmajo ambaye alipata kura 110.

 

Wabunge watatu waliripotiwa kuharibu kura zao. Kiongozi wa zamani wa taifa la Somali Hassan sheikh Mohamud amechaguliwa kuwa rais baada ya kura ya mwisho ilioshirikisha wabunge pekee.

 

Alimshinda rais aliyepo madarakani Mohammed Abdullahi farmajo ambaye amekuwa akihudumu tangu 2017.

 

Hali hiyo inamulika suala la ukosefu wa usalama nchini Somalia Pamoja na ukosefu wa uwajibikaji wa kidemokrasia.

 

Matokeo hayo yanaadhimisha kurudi kwa Hassan Sheikh Mohamud , aliyehudumu kati ya 2012 hadi 2017 kabla ya kushindwa na Farmajo.

 

Uchaguzi huo - ambao ulikuwa na ushindani mkali na ambao uliingia katika raundi ya tatu - ulicheleweshwa kwa takriban miezi 15 kutokana na vita na masuala ya usalama.

 

Bwana Mohamud aliapishwa muda mfupi baada ya matokeo ya mwisho kutangazwa , na kuwafanya wafuasi wake katika mji huo kumpongeza mbali na kufyatua risasi hewani . Atahudumu kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

 

Katika uchaguzi huo wa Jumapili , mamia ya wabunge walipiga kura zao katika anga moja ya ndege katika mji mkuu wa Mogadishu.

 

Milipuko ilisikika karibu na eneo hilo huku uchaguzi ukiendelea lakini maafisa wa polisi wanasema kwamba hakuna mtu aliyejeruhiwa.

 

Akiwa rais mtarajiwa, bwana Mohamud atalazimika kukabiliana na athari za ukame ambapo Umoja wa mataifa unasema kwamba takriban raia milioni 3.5 wako hatarini kukumbwa na kiangazi cha kiwango cha juu.

 

Lakini jukumu kuu analokabiliana nalo ni kukomboa eneo kubwa la taifa hilo ambalo lipo chini ya udhibiti wa kundi la wapiganaji wa Alshabab.

 

 

Uchaguzi huo ulifanyika katika anga moja katika uwanja wa ndege wa Somalia

 

Kundi hilo linaloshirikiana na lile la al-Qaeda linaendelea kudhibiti maeneo makubwa ya taifa hilo na limekuwa likitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara mjini Mogadishu.

 

Taifa hilo pia linaathiriwa na ukosefu wa chakula na mafuta kutokana na mfumuko uliosababishwa na vita vya Ukraine.

 

Je uchaguzi huo ulifanyikaje?

Uchaguzi huu ulitarajiwa kufanyika mwaka uliopita wakati muhula wa miaka minne wa bwana farmajo ulipokamilika. Lakini tofauti za kisiasa na ukosefu wa uthabiti ulichelewesha kura hiyo huku rais aliyekuwa akihudumu akisalia madarakani.

 

Wabunge waliomchagua rais mpya wao wenyewe walichaguliwa na wajumbe waliochaguliwa na jamii za taifa hilo.

 

Walikusanyika katika anga kubwa ya ndege katika kambi ya Halane yenye ulinzi wa hali ya juu. Hii ndio kambi kuu ya wanajeshi wa muungano wa Afrika nchini Somalia{Atims}, Pamoja na nyumbani kwa mabalozi wengi na mashirika ya misaada.

 

Upigaji kura , uliofanyika kwa kura ya siri , ulicheleweshwa kwa saa kadhaa kutokana na ukaguzi wa muda mrefu.

 

Chaguzi za awali ziliathiriwa na madai ya ununuzi wa kura huku wagombea wakitoa fedha ili kupata uungwaji mkono.

 

Mgombea wa pekee , aliyekuwa Waziri wa masuala ya kigeni Fawzia Yusuf Adaa, aliondolewa katika raundi ya kwanza ya uchaguzi huo.

 

Je al-Shabab imesemaje?

Katika chaguzi zilizopita , al-shabab ilitishia na hata kuwateka nyara baadhi ya viongozi wa koo kwa kuwashutumu kwa kushiriki katika kile ilichokitaja kuwa uchaguzi usio wa kiislamu.

 

Wakati huu, kundi hilo halikutoa tamko lolote kuhusu uchaguzi huo, huku kukiwa na hofu kwamba wanachama wake huenda walichaguliwa kisiri katika bunge la taifa hilo ili kukandamiza serikali wakiwa ndani.

 

Hofu ilioneshwa wazi na rais wa Djibout Omar Guelleh mwaka 2020, aliponukuliwa akisema: Nina hofu kwamba tutasalia na bunge linalodhibitiwa na kundi la al-Shabab, kwasababu watanunua uungwaji mkono wa baadhi ya wabunge.

 

Baadhi ya wachanganuzi walihisi kwamba bwana Guelleh alikuwa akichochea uwezekano wa kundi hilo kushiriki katika bunge , lakini hakuna tashwishi kwamba lina uwezo mkubwa kisiasa nchini Somalia.


Kinglayz Wakuchana

378 Blog posts

Comments