Simuulizi ya kuelimisha jamii

Penzi la johali nisimulizi nzuri yenye kuelimisha jamii

Simulizi............PENZI LA JOHARI

Mtunzi...............Official Dully

WhatsApp....0628924768

Mkasa......wa....kutisha

 

           Sehemu Ya {01}

 

   Kiza kilikuwa kimetanda, hali ya hewa ilikuwa ya upepo mkali ambayo ilipelekea baadhi ya miti mikubwa kuanguka, upepo huo haukuwa wa kawaida maana ulivuma bila kukoma na kupelekea miti kupata tabu usiku wa siku hiyo.

      Hali ya mawingu ilianza kubadilika, ngurumo za radi zilianza kupiga kwa nguvu sana na hii ilionesha kuwa wakati wowote na saa yeyote mvua kubwa itashuka.

 

Muda ulisomeka ni saa nane usiku, lakini wakati upepo bado unaendelea kuvuma na radi kupiga ghafla mvua kubwa ilianza kunyesha, mvua iliyosindikizwa na radi pamoja na upepo mkali ambao uliendelea kuangusha miti mikubwa sana..

 

"Msaadaaaa, nakufaaaa..!!!"

 

Wakati mvua inaendelea kunyesha na ngurumo za radi kuchukua nafasi yake ghafla ilisikika sauti ya kiume ikiomba msaada na muda si punde alionekana kijana wa makamo akikimbia huku akiwa mwingi wa hofu na wasiwasi mkubwa sana.

 

Haikufahamika ametokea wapi na alikuwa akikimbizwa na nani lakini kwa jinsi alivyokuwa akikimbia na hofu iliyokuwa nayo basi ilionesha alikuwa kwenye hatari kubwa sana.

 

"Ha.ha.ha.ha..unafikiri utakimbia mpaka wapi, wewe ni wetu sasa na lazima damu yako imwagike kwahiyo uwe mpole tu kijana"

      Sauti nzito iliyojaa mikwaruzo ilisikika na kumfanya yule kijana aanguke chini na kuziba masikio yake ambayo yalikuwa yakitoa damu na hii ilionesha jinsi gani ile sauti ilikuwa ikimdhuru.

 

"Tafadhali...naomba mniache niende, sina kosa lolote ambalo nimewakosea tafadhali naombeni mniache jamani.!!"

    Yule kijana alizungumza kwa sauti iliyojaa hofu lakini wakati anazungumza hayo alitokea mtu mrefu sana na kusimama mbele yake.

 

Haikufahamika alikuwa ni nani lakini mtu yule alikuwa ni wa ajabu sana ambae alichanganya uhalisia na kiumbe wa kutisha. Alikuwa mwenye manyoya mwili mzima, kucha ndefu na meno makali sana kinywani mwake.

    Si hivyo tu pia alikuwa na mkia mrefu sana ambao ulijaa manyoya yenye kuwaka mithiri ya dhahabu na kufanya upendeze sana kuutazama.

 

"Huwezi kuachwa kuishi kamwe, unatakiwa kufa na baada ya kifo chako amani itatawala ndani ya jamii yetu"

     Alizungumza yule kiumbe kwa sauti iliyozidi kumuumiza yule kijana lakini mwisho nguvu zilimuisha na kupoteza fahamu papo hapo.

 

Alikuja kuzinduka baadae sana akiwa kwenye jiwe kubwa sana, jiwe ambalo lilikuwa na harufu ya kifo na pembeni kwa jiwe hilo yalizunguka madimbwi ya damu na hii ilimfanya yule kijana atambue alikuwa kwenye jiwe la kutolea kafara.

     Alijaribu kujiinua lakini alishindwa, mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa kwa kamba ambayo ilimzuia kufanya chochote cha kujinasua hapo.

 

Alihangaika sana lakini mwisho alikata tamaa na kutulia, alichosubiri ni kufa na sio kingine. Yalipita masaa kadhaa na ilipotimu saa 11 karibu na kupambazuka ndipo alifika tena yule kiuambe akiwa na jopo la wenzake ambao kwa muonekano hawakutofautiana sana.

 

Baada ya kufika walimsogelea na kumzunguka, wawili walikamata mikono yake na wawili walikamata miguu yake kisha mmoja alikamata kichwa na yule aliemleta hapo alisogea akiwa na kisu kikali mkononi mwake.

 

Hakukuwa na matumaini ya kuishi tena kwa kijana huyo ila ni dua pekee za kumuomba Mungu ampokee ndizo zilikua zikitamkwa kwenye nafsi yake.

 

Usiku huo ulikuwa ni usiku wa kutisha sana ulikuwa ni usiku wa mwisho kwa kijana huyo kuuona ulimwengu hivyo kufumba na kufumbua kichwa chake kilikuwa chini na damu tu ndizo zilikuwa zikiruka na kutapakaa kila mahali.

 

                       *******

 

Ilikuwa ni ndoto ya kutisha sana kwa kijana huyo ambayo ilimfanya akurupuke kutoka usingizini na kujikuta akitetemeka kwa hofu.

 

"Ni ndoto gani tena hii jamani, mbona inatisha kiasi hiki.!!?"

     Alizungumza kijana huyo ambae taratibu alishuka kutoka kitandani na kusogea mezani ambapo alichukua simu yake na kupiga mahali.

 

Kulikuwa tayari kumepambazuka, yapata kama majira ya saa mbili asubuhi, baada ya kupiga simu iliita kidogo mwisho ilipokelewa na sauti ya kiume ilisikika upande wa pili.

 

"Nambie Jimmy.?"

 

"Nikwambie nini ndugu yangu yaani hata sielewi kila siku afadhali ya jana.!!"

 

"Kwahiyo unataka kusema leo tena umeota ile ndoto ya kutisha.!?"

 

"Jeremiah yaani acha tu alafu unajua tangu nilivyoenda kutembelea makaburi ya wazazi wangu ndiyo ndoto hizi zimeanza kuniandama, inafika wakati mpaka nauchukia usiku"

 

"Daaah pole sana ila yatakwisha hayo, najua labda itakuwa mizimu ya wazazi wako imekukasirikia maana tangu wamefariki hukuenda hata kufagilia makaburi yao ila nahisi ni adhabu hiyo wanakupa lakini usijali mambo yatakuwa sawa Jimmy."

 

"Ok sawa ila jiandae basi twende kazini unajua tumechelewa sana nahisi wateja wanatusubiri"

    Alizungumza Jimmy na kukata simu kisha aliingia bafuni kuoga na baada ya dakika kadhaa alirudi ila alipotazama kitanda chake alishangaa kukuta kimetapakaa damu na kumfanya aingiwe na hofu sana.

 

"Mungu wangu..!!"

     Jimmy alihamaki, hakutaka kuendelea kubaki humo, haraka alitoka mpaka sebuleni na kusimama huku akitafakari ni nini ameona au huenda ikawa ni wasiwasi wake.

 

Alikaa akitafakari kwa takribani saa nzima lakini mwisho aliona huenda utakuwa ni wasiwasi wake hivyo alijongea taratibu na kuingia chumbani kwake lakini ajabu hakuona zile damu alikuta kupo kawaida sana na hapo akaamini huenda ulikuwa ni wasiwasi wake kweli.

 

Alijiandaa vizuri na baada ya kumaliza alitoka mpaka nnje, alipanda gari yake na kuanza safari lakini muda wote alikuwa akiikumba ile ndoto na kumuumiza kichwa sana.

 

"Hua naota ndoto nyingi sana za kutisha lakini hii ya leo imezidi, au kuna jambo baya linaenda kutokea mbele yangu maana watu husema ndoto hua zina ukweli sasa ukweli wake ni upo au imenitabiria nini.!?"

 

Hakuna jibu maaluma alilipata Jimmy lakini alipotezea na baada ya mwendo mrefu alifika kazini kwake ila alipofika na kushuka kwenye gari alifika binti mmoja na kusimama mbele yake.

 

"Habari yako bosi?"

 

"Salama Asha nambie wateja tayari wamefika au bado maana leo nimechelewa sana kufika"

 

"Bado hawajafika ila walipiga simu wamesema watachelewa kidogo kwahiyo tuwavumilie"

 

"Ok aina shida"

     Jimmy alipiga hatua kadhaa kuelekea ofisini kwake lakini Asha alimwita na alipogeuka Asha alisogea mpaka karibu yake huku akiwa mpole sana.

 

"Lakini bosi leo wakati nafika na kufungua ofisi kuna dada mmoja nimemuona ameketi hapa nnje sasa kila nikimuuliza nimsaidie nini hanijibu kitu zaidi ya kutabasamu tu"

 

"Sasa kwahiyo umemfukuza au.!?"

 

"Hapana nimemkaribisha yupo ofisini kwangu nimeona nisimfukuze huenda akawa anahitaji kuongea na wewe kwahiyo nimemkaribisha"

 

"Ok mlete ofisini kwangu"

      Jimmy alijongea mpaka ofisini kwake, alivua koti lake na kuliweka juu ya kiti sehemu ya kuegamia kisha aliketi na muda huo huo mrango wa ofisi yake ulifunguliwa, aliingia Asha akiongozana na binti ambae hakufahamika ametokea wapi.

 

"Bosi binti mwenyewe ni huyu"

      Alizungumza Asha na Jimmy alitoa amri yule binti aketi kwenye kiti kwaajili ya mazungumzo afahamu ametokea wapi na shida yake ni nini mpaka kufika hapo.

 

"Asha unaweza kwenda kuendelea na majukumu yako"

 

"Sawa bosi"

 

Asha hakuwa na sababu ya kuendelea kubaki hapo, alitoka nnje na kumuacha Jimmy akimtazama yule binti na kumtathimini maana muonekano wake wa mavazi ulitosha kumueleza ni mtu mwenye maisha magumu sana.

 

Nguo alizovaa zilikuwa chakavu sana zilizotoa harufu ya jasho, nyewe zilikuwa hazina ushirikiano hakuwa na tofauti na mtu aliepungukiwa akili au kichaa.

 

"Samahani dadaangu unaitwa nani na umetokea wapi.!?"

     Jimmy alimuuliza yule binti lakini yule binti alionekana ni mtu mwenye kufikiria huenda jina lake alikuwa amelisahau au amepoteza kumbu kumbu.

 

"Na..na..naitwa Johari"

      Alijibu huku macho yake yakizunguka kutazama pande zote za ofisi ile.

 

"Oh Johari sasa unaweza kuniambia umetokea wapi?"

      Jimmy alimuuliza Johari lakini hakupata jibu na muda huo tumbo la Johari lilianza kuunguruma kuashiria alikuwa na njaa.

 

Basi jimmy hakutaka kuendelea kumuhoji maswali, aliinuka na kutoka nnje, baada ya dakika kadhaa alirudi akiwa na kifungua kinywa pamoja na maji.

     Alimpatia na Johari kwakua alikuwa na njaa sana alivifakamia kwa haraka na alipomaliza hakutaka kushukuru aliinuka na kutoka zake nnje, kitendo ambacho kilimfanya Jimmy ashangae sana.

 

                     ************

 

Upande wa pili kwenye sayari ya mbali, kwenye ulimwengu mwingine walionekana mabinti wawili wamepiga magoti mbele ya mfalme sambamba na malkia na walionesha kuwa wenye huzuni sana, huzuni iliyopelekea macho yao kudondosha machozi.

 

"Tafadhali baba tusamehe lakini Johari mwenyewe ndiye aliomba tutoke na kwenda kwenye sayari ya binaadamu hivyo wakati wa kurudi tulipotea nae na hatujui wapi alipo.!!"

      Aliongea binti mmoja kati ya wale mabinti wawili waliopiga magoti mbele ya mfalme.

 

"Mnajua kabisa majini na binaadamu si rafiki, na niliwakataza kabisa kwenda sayari ya binaadamu lakini mmeonesha kiburi na madhara yake ni haya mdogo wenu amepotea na hatujui kama ni mzima au laa..!!!!"

 

"Lakini baba....!!"

 

"Sitaki muongee tena, walinzi hebu chukua hawa wawekwe chumba cha kiza wasitoke mpaka Johari akipatikana"

     Amri ya Mfalme ilitolewa na wale mabinti wawili walichukuliwa huku wakilia na kuomba wasamehewe lakini Mfalme hakutaka kuwasikia na Malkia muda wote alikuwa akilia kwa kumpoteza binti yake ambae hawakujua ni mzima au laa.

 

Mfalme aliita vijana wawili na lengo la kuwaita ni kuwatuma kwenye sayari ambao wanaishi binaadamu ili kwenda kumtafuta Johari kumrudisha kwenye ulimwengu wao wa majini.

 

"Vijana nafikiri mnajua kuwa hivi karibu Johari anatakiwa kuolewa kwahiyo basi nataka muende kwenye sayari wa binaadamu, hakikisheni mnarudi na Johari hapa la sivyo msirudi na mfie huko huko, na kama kuna kizuizi chochote au kuna binaadamu yeyote yupo karibu nae hakikisheni mnamuangamiza"

 

"Sawa mtukufu mfalme tumekuelewa na tunaahidi kazi itakamilika lazima turudi na Princess Johari akiwa mzima"

 

Vijana walimtoa hofu mfalme na baada ya kuruhusiwa walianza safari kuelekea kwenye ulimwengu wa wanadamu ambapo ndipo Johari amepotelea na huenda ingechukua takribani mwezi mzima kufika kwenye ulimwengu wa binaadamu na kuanza jukumu lao.

 

Upande wa Jimmy baada ya Johari kupata kifungua kinywa na kutoka nnje nae alitoka kwa lengo la kumuuliza maswali ili kumjua kiundani zaidi pasi na kufahamu alikuwa akimfuata kiumbe hatari ambae kama akiweka ukaribu nae basi huenda ikagharimu maisha yake na kubaki jina tu....ITAENDELEA....

 

- Nini kitafuata, Johari atapatikana kweli na vipi kuhusu mauzauza anayokutana nayo Jimmy mwisho wake ni nini maana mambo ndiyo kwanza yanaanza...

 

Kupata simulizi hii mpaka mwisho, kwa wakati na kwa mtiririko sahihi basi hakikisha ume like na kufollow page yetu kwa kugusa link hapo chini?

 

https://m.facebook.com/StoryMpya


Naomi essau

100 Blog posts

Comments