Serikali ya Taliban imekataa wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kuondoa vikwazo vikali vilivyowekwa dhidi ya wanawake wa Afghanistan. Taliban imepuuzia mbali wito huo ikisema hauna msingi.
Baraza la Usalama liliunga mkono kwa kauli moja azimio ambalo liliikosoa serikali ya Taliban kwa kuwawekea vizuizi wasichana na wanawake kupata elimu, kazi za serikali na uhuru wa kutembea tangu walipotwaa madaraka mwaka jana.
Kiongozi mkuu wa Afghanistan Hibatullah Akhundzada pia amewaamuru wanawake kujifunika -- zikiwemo nyuso zao -- wakati wakiwa katika maeneo ya umma, hatua iliyozusha ukosoaji wa kimataifa.
Wizara ya Mambo ya kigeni ya Afghanistan imesema kwa sababu watu wa nchi hiyo wengi wao ni Waislamu, serikali ya Afghanistan inazingatia muongozo wa utamaduni na sharia za kiislamu.