JANGA la Covid-19 na ambalo lilitua nchini Machi 202 limeathiri karibu kila sekta. Kuanzia sekta ya afya, usafiri na uchukuzi, elimu, ile ya utalii na hoteli ikiwa iliyoathirika zaidi. Wanaofanya biashara ya ngono pia hawajasazwa.
Huku wengi wakijipata kuacha biashara hiyo, kulemewa na msongo wa mawazo na kuishia kutumia dawa za kulevya na mihadarati, baadhi wametafuta “njia mbadala kuendeleza kazi hiyo ya tangu zamani ulimwenguni.”
Makahaba katika Kaunti ya Tana River wamejumuisha huduma za usafi wa nyumba, kwenye biashara yao.Kwa sasa, wanaendeleza huduma zao nyumbani badala ya mitaani.Si siri, hatua hiyo ina malipo ya kuridhisha, wanaiambia Taifa Leo Digitali.
“Mbinu sasa imebadilika. Wateja tunawahudumia kama wachumba wetu. Biashara imenoga,” anasema Anne Syokau, akiongeza kuwa malipo ni bora.Mbali na biashara yao halisi, wamejuisha kufulia wateja nguo, mapishi na kuwanyoosha viungo vya mwili katika makazi yao.
“Wengi wa wateja wetu ni makapera, watumishi wa umma, wafanyabiashara wa mijini na wanaume walio kwenye ndoa na wanaohitaji huduma zetu,” Anne anafichua.
Mapato kupanda
Huduma hizo kijumla hazipungui Sh2, 000, mapato ambayo makahaba hao wanaridhia, yakilinganishwa na ratiba ya kawaida mitaani na ambayo malipo yake ni ya chini.Wateja wanaoridhika, hulipa vyema, baadhi yao wakiomba mahusiano wa kipekee.
“Si kama kitambo ambapo tulikuwa tukikodi lojing’i ama kutoa huduma kwenye veranda, kona ya majengo, maeneo yenye baridi.“Awali, baadhi ya siku tungelala usiku kucha kwenye baridi bila kupata wateja na kurudi nyumbani bila mapato,” anasimulia Milcah Achieng.
Ujanja huo umechangia usalama wao kuimarika. Wanasema kwa sasa wamekwepa kero ya maafisa wa polisi, wanaohoji wamekuwa wakivuna hela za bwerere, “mashamba ambayo hawakufanya upanzi”.Isitoshe, wanasema gharama katika nyumba zao imepungua kwa sababu wateja wao wananua chakula na pia kitanda bora.
“Kwa wiki huunda zaidi ya Sh10, 000. Ukiimarisha uhusiano bora na wateja, si ajabu kuingiza kima hicho cha mapato chini ya siku chache,” Achieng asema.Aidha, baadhi ya makahaba wamegura biashara hiyo mitaani, na kuanzisha uchumba na baadhi ya wateja wao.
Wametambua wanaume wa kujishirikisha na uchumba wa karibu.Cicily Maingi anasema anapanga kufunga pingu za maisha, kufikia mwishoni mwa mwaka huu, 2021.
Kuacha uhakahaba
“Amenipendekezea posa mara mbili, anataka niwe mke wake wa pili kwa sababu mke wake wa kwanza hana mtoto. Mkewe amekubali, ila mama yake (mama wa mume) amekataa. Ninaendelea kutathmini ombi lake,” mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 24 anaelezea.
Wawili hao watasafiri mashambani kujadiliana na wazazi wa jamaa.Maingi hatimaye huenda akagura biashara ya ukahaba.Baadhi ya wanaume wanaridhia huduma za nyumbani, wakizisifia kuwa bora na nafuu.
John Emase anasema anaokoa kiasi kikubwa cha pesa anapopeleka mwanamke anayempikia nyumbani, kama mojawapo ya baadhi za huduma.“Ninachofanya ni kununua chakula na sabuni ya kufua nguo. Hatua hiyo inaniokolea zaidi ya Sh1, 500 kila wiki,” anaiambia Taifa Leo Digitali.
Emase anapendekeza makahaba waache kuendesha biashara yao mitaani, na kuilekeza maeneo ya faragha kwa sababu inawaondolewa kukosewa heshima.Hata hivyo, mwanaharakati Jemimah Wangari anasema huduma za nyumbani huenda zikawa chocheo la ndoa nyingi kusambaratika.
“Baadhi ya wanawake hao wanataka kuoleka na waume wa wenyewe, kisiri. Kuna uwezekano wakawageuza vikaragosi kukamua hela,” Wangari anaonya.Mwanaharakati huyo anatahadharisha kilele hilo kitakuwa wanaume kuasi ndoa zao na majukumu ya familia, na ndoa kusambaratika.
Ni mkondo unaotarajiwa kuwa na mkengeuko wa mambo mengi, janga la Covid-19 likiendelea kuchangia mabadiliko.Huduma za mitaani zinaendelea kufifia, wanawake waliooneka kuvalia vibiriti ngoma wakipungua.