3 yrs - Translate

MY CHOICE
(chaguo langu)
By: Iddi Manjawila
Watsap; +255787864849

~sehemu ya1~

Utangulizi:

Kusema neno nakupenda haitoshi kuelezea hisia zangu kwako, hivyo natoa machozi ili yazidi kuelezea maumivu nipatayo ndani ya moyo wangu juu yako.
Wacha matendo yangu yaongee maana mimi mwenzio ni dhaifu sana kwako, yaani kilichomo moyoni mwangu siwezi kukielezea mdomoni mwangu.
Hakika mapenzi ni hisia kali sana ambazo zinaumiza lakini hazichoshi, tumekutana kwa bahati mbaya, ila kamwe siwezi kujutia kukupenda wewe, kwani wewe ndio CHAGUO LANGU..
'MY CHOICE'

~*******~

BATAZARI ni kijana ambae amepoteza wazazi wake wote wawili baada ya kukatwakatwa na mapanga kufuatia na migogoro iliyokuwepo kati ya wakulima na wafugaji huko mkoani Morogoro.
Baada ya kifo cha wazazi wake Batazari alikosa kabisa ndugu wa kuwategemea kwani ndugu zake wote walishauwawa na wafugaji ambao ilisemekana kuwa ni jamii ya kimasai, hivyo msaada pekee uliokua umebaki kwa kijana Batazari ni kutoka kwa babu yake mzaa mama Mzee Mtupa ambae naye alikua akiishi mkoa wa Tanga, na huko ndipo Batazari alipoamini atapata msaada wa maisha yake.
Kweli, baada ya siku kadhaa Batazari alifika kwa babu yake mkoani Tanga na kuanza maisha mapya.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo, Batazari alifunsishwa na babu yake mambo mengi sana yanayohusu shughuli za uvuvi, na hatimaye Batazari akawa na uwezo mkubwa sana wa kuvua samaki bila hata ya kutemea msaada wa babu yake, wakati huo alikua na miaka ishirini na tatu.
Kijana Batazari alijulikana sana na wauzaji wa samaki hasa wale waliopo maeneo ya sokoni, hii ni kutokana na tabia njema pamoja nidhamu aliyokuanayo kijana huyu, pia kutokana na uaminifu wake Batazari, ni sifa ya ziada iliyomfanya awe na idadi kibwa ya wateja wa samaki wake baada ya Kuvua kutoka baharini.
Baada ya siku kadhaa kupita hali ya kiafya ya babu yake Batazari mzee Mtupa ilianza kudhoofika..

Mzee Mtupa akaanza kupunguza safari zake za kwenda baharini, lakini mwisho aliona ni vyema apumzike nyumbani kwani itamletea madhara makubwa siku moja, hivyo alimuachia majukumu yote ya uvuvi pamoja na majukumu ya nyumbani mjukuu wake Batazari.

Ilikua ni asubuhi ya saa kumi na mbili ambapo jua halikupata nafasi ya kuchomoza siku hiyo kufuatia na kufunikwa na mawingu ya mvua huku vinyunyu vya mvua vikidondoka maeneo ya baharini, hali hii ilitokana na mvua kubwa sana iliyonyesha usiku wa kuamkia siku hiyo.
Wavuvi wengi sana hawakuweza kufika baharini siku hiyo, ni kijana Batazari pekee ndiye aliyefanikiwa kufika katika bahari hiyo, ambapo kama kawaida yake aliweka nanga mtumbwi wake baada ya kutoka katikati ya bahari kuvua samaki, Batazari alishuka kutoka katika mtumbwi huo huku akiwa ameshika kapu kubwa ambalo alikua amelijaza samaki, akaanza kutembea kuelekea ufukweni ambapo ndipo alipohifadhi nguo zake katika miti aina ya mikoko iliyopo pembezoni kidogo mwa ufukwe wa bahari hiyo.
Akiwa kama umbali wa mita kadhaa kabla ya kufika ufukweni, ghafla Batazari alimuona mtu akiwa amelala katika ufukwe wa bahari hiyo huku akiwa amevaa lifejacket na alikua akionekana kusukumwasukumwa na mawimbi ya bahari hiyo.
Batazari alikimbia kutoka baharini hadi ufukweni ambapo alifanikiwa kuona ni nani aliyekuwa ameletwa na mawimbi ya bahari pale ufukweni.
Ooh.! Mungu wangu..! Hakika alikua msichana mzuri sana ambae Batazari hakuwahi kumuona kabla, ila kutokana na misukosuko ya mawimbi ya bahari mwili pamoja na sura yake vilikua na uvimbe kidogo.
Batazari alijiuliza maswali kadhaa baada ya kugundua kuwa msichana yule alikua ni mzima na alikua akihitaji msaada, hakujua amsaidie vipi ila ghafla akakumbuka baadhi ya mafunzo na maelekezo aliyowahi kupewa na babu yake, kuwa kwanza ni kumkamua maji pamoja na kumsaidia pumzi mtu aliyezidiwa na maji.
Hivyo Batazri alianza kumkamua maji yule msichana kwa kumbinyabinya tumboni mwake, baadae akagusanisha midomo yake na midomo ya yule msichana kwa lengo la kumsaidia pumzi, alifanya hivyo kama mara kadhaa mpaka yule msichana akaanza kukohoa, Batazari aliendelea kutoa huduma hiyo mpaka yule msichana akaanza kufumbua macho na hatimaye kuamka na kuanza kupumua mwenyewe bila msaada wa Batazari.

Batazari alimbeba yule msichana mpaka kwenye miti ya mikoko ambapo yeye ndipo anapoweka kambi yake kabla ya kuingia baharini kuvua samaki, walikaa hapo kama muda wa nusu saa hivi ambapo Batazari alipika uji katika kisufuria kidogo ambacho yeye mwenyewe huwa anakitumia kisufuria hicho kwa kupikia ugali.
Alimpa yule msichana uji na alipomaliza kunywa uji na kuhakikisha ameshapata nguvu hata ya kuongea, ndipo Batazari alianza kumuuliza yule msichana kuwa ni nini kilimpata mpaka akamkuta pale ufukweni tena akiwa katika hali ile ya karibu na kufa.

Yule msichana alieleza kuwa yeye hana kumbukumbu vizuri juu ya maisha yake ya nyuma, ila anachokikumbuka kwa sasa ni kuwa yeye ni mwandishi wa habari ambae alipata taarifa kuwa kuna meli imekamatwa na polisi ambayo ilikua imebeba madawa ya kulevya, meli hiyo ya mizigo ilikuwa imekamatwa maeneo ya Pemba karibu na mkondo wa bahari ya Tanga, hivyo ilimbidi yule msichana akodi boti ya haraka ili awahi kupiga picha pamoja na kuripoti tukio hilo live katika televisheni kabla ya vyombo vingine vya habari kupata taarifa hiyo.
Msichana aliendelea kwa kusema kuwa, wakiwa njiani karibu na eneo la tukio, ndipo ghafla bahari ikachafuka, alisema ilikua ni saa sita mchana lakini ghafla kiza kilianza kutanda na kuwa kama usiku katika eneo lile, boti yao ilizima ghafla na kupigwa na kurushwarushwa juu na mawimbi ya bahari ile, mara ghafla ukaja upepo mkali mno huku ukiambatana na radi kali sana, mvua kubwa ikaanza kunyesha huku upepo ukizidi kuikokota boti yao na kuibadilishia muelekeo.
Kwa bahati nzuri yule msichana aliwahi kuvaa lifejacket na kujitupa baharini, hata hivyo maji yalimzidi na kumshinda nguvu kabisa, hatimaye akapoteza matumaini ya kuishi tena baada ya kuishuhudia boti yao ikizama mbele ya macho yake, akahisi kifo kipo mbele yake, sasa ndio anashangaa hata yeye hajui ni miujiza gani ilitokea mpaka yeye akaokoka tena katika mji mwengine kabisa.

Batazari alimuonea huruma sana yule msichana, na alimpa pole pamoja na kumuomba awe na subira kwani mwenyezi Mungu anasababu ya kumuokoa kutoka kwenye kifo.
Baada ya muda wa kama nusu saa kupita tangu walipomaliza maongezi yao, Batazari alimwambia yule msichana kuwa kwanza waelekee nyumbani wakapate ushauri kutoka kwa babu juu ya nini cha kufanya..

Itaendelea..!

Mungu awabariki na nawapenda sana..

image

Install Palscity app