Ukosefu wa mvua kwa kipindi kirefu katika eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi umezua wasi wasi miongoni mwa wakazi huku wakihofia kukumbwa na baa la njaa.
Wakizungumza na mwanahabari wetu katika eneo hilo wenyeji hao wakiongozwa na David Bakari wamesema wameanza kushuhudia mabadiliko ya hali ya anga na hawana matumaini ya kushuhudia mvua na huenda baadhi yao wakapoteza maisha kufuatia makali ya njaa kwani tayari wale walioenda mijini kutafuta ajira wamelazimika kurudi mashinani baada ya janga la Korona kuathiri kazi zao.
Aidha sasa wanaitaka serikali ya kaunti ya Kilifi kuingilia kati na kuhakikisha kuwa wanapata mwafaka wa suala hilo kwa wakazi na taasisi za elimu zilizoko katika eneo hilo kwa kuanzisha mpango wa chakula kwa wanafunzi kama ilivyokuwa hapo awali.
Kwa upande wake msimamizi wa wadi ya Sokoke katika kaunti ndogo ya Ganze James Muye amethibitisha swala hilo huku akisema kuwa tayari serikali ya kuanti hii imechukua takwimu ili kuwawezesha kukabiliana na njaa kupitia idara ya Majanga kaunti ya Kilifi.